WANDISHI KIGOMA WAOMBWA KUWAHABARISHA WANANCHI JUU YA KAMBI YA KIBINGWA MAWENI RRH
Posted on: May 23rd, 2025
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni - Kigoma leo tarehe 24 Mei,2025 imefanya mkutano na Waandishi wa Habari kwa lengo la kuwajulisha ujio wa kambi ya matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi.
Katika mkutano huo ambao umefanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni - Kigoma Dkt. Joseph Nangawe Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali amewaomba wandishi kufikisha ujumbe kwa jimii ili waweze kutambua fursa hiyo ya matibabu.
"niwaombe nyote Waandishi wa Habari kuwa mabalozi wa taarifa hizi muwahabarishe wananchi kwa nguvu zote kuhusu fursa hii muhimu, kwa pamoja tunaweza kuhakikisha ujumbe huu unawafikia wananchi kwa urahi" amesema Nangawe, Kaimu Mganga Mfawidhi.
Pia kaimu Mratibu wa Huduma za Afya Dkt. Ashrafu I. Bitaliho amesema kutokana na takwimu za kila siku kambi hii inatarajia kuwahudumia wananchi 2000 ndani ya siku tano ambapo pia amewaomba Waandishi wa Habari kufikisha ujumbe kwa wananchi.
"Kutokana na takwimu za kila siku katika utoaji wa huduma ni kwamba maeneo haya ambayo yameguswa yamekua na namba kubwa ya wagonjwa kuliko mengine hivyo kama Hospitali tumeona nieneo sahihi kulifanyia kazi hasa katika kuwahudumia wananchi. amesema Dkt. Ashrafu.
Hata hivyo Dkt Nangawe ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kutumia fursa hii huku akitoa shukrani kwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mh.Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuboresha hospitali za Mikoa ikiwemo Hospitali ya Mkoa Maweni-Kigoma.