WANANCHI ZAIDI YA 1200 KUPATIWA HUDUMA NDANI YA SIKU TANO MAWENI RRH KIGOMA
Posted on: May 26th, 2025
Leo tarehe 26 Mei, 2025, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni -Kigoma imezindua Rasmi kambi ya matibabu ya kibingwa na bingwa bobezi yenge lengo kuwasogezea huduma na kuwapunguzia gharama wananchi huku wananchi 1200 wakitarajiwa kuhudumiwa ndani ya siku tano.
Katika uzunduzi huo ambao umefanywa na Generali Mstaafu wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji Mh. Thobias Andengenye, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma amewataka wananchi kutumia fursa ya uwepo wa madakitari Bingwa na Bobezi kupata huduma ambazo zimekuja kupunguza gharama kuzifuata katika hospitali za mbali kama Bugando Mwanza, Muhimbili na nyinginezo.
“Sote tunatambua kuwa kuwapata wataalamu wa Afya siyo kazi nyepesi lakini Serikali yetu inafanya jitihada ili kufikisha huduma hizi kwa wananchi hasa kwa njia za ubunifu kama inavyofanya Hospitali yetu ya Rufaa ya Maweni, tumekua tukizifuata huduma hizi Mikoa mbalimbali yenye hospitali kubwa ambapo ni gharama laikini pia nimbali hivyo hii kambi imekuja kupunguza gharama na kusogeza huduma mkoani kwetu. Amesema Mh. Andengenye, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.
Akiendelea kuongea na wananchi katika uzinduzi huo Mh. Andengenye amewataka madaktari Bingwa na Bobezi kuendelea kuitikia wito na kuwsaidia wananchi huku akiwakumbusha wananchi kushiriki katika uchaguzi ili kuweza kupata viongozi wenye maono na kuendelea kuwahudumia wananchi.
“Kwa wananchi mlioko hapa niendelee kuwahimiza tushiriki uchaguzi ili kuweza kupata viongozi wanaoweza kuleta maona kwani haya yanayofanyika hayaji tu, bali kunamtu ambaye ameshikilia maono hayo kwahiyo niwaombe sana kila mmoja aweze kushiriki” amesema Mh. Andengenye.
Hata hivyo Mh. Hassan Rugwa, Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma amesema kilicho fanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni -Kigoma ni kitu kikubwa kwani wataalamu wote waliokuja kutoa huduma imekuja kupunguza gharama kwa wananchi kwani siyo wananchi wote wanaweza kusafiri kuzifikia huduma mbali na maeneo yao.
“Natambua changamoto kubwa tuliyonayo ya madaktari Bingwa na Bobezi hivyo tunamshukuru Mh.Dk.Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutuletea timu hii ya madakitari Bingwa hapa, hii inaenda kupunguza gharama kwasababu siyo watu wote hapa wangeweza kusafiri Kwenda nchi au Mikoa mingine kupata huduma hizi” amesema Mh. Rugwa, Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma.
Kwa upande wake Bw. Rukas Machibya, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Hospitali ameushukuru uongozi wa Mkoa kwa ushirikiano ambao umekua ukiutoa katika kuhakikisha huduma za Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni zinatolewa kwa wananchi ambapo umekua ushirikiano wenye tija katika utoaji wa huduma.
“Kwanza kabisa nipende kutoa shukrani kwako Mh. Mkuu wa Mkoa na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa iliyoko chini yako kwa ushirikiano ambao mmekua mkiutoa kwetu, kwakweli umeleta na unaendelea kuleta tija katika kuwahudumia wananchi” amesema Machibya.
Pia baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Kigoma wemesema kuwa wanafuraha sana kuwepo kwa madaktari Bingwa kwani wanaamini kuwa wanaenda kupata huduma bora.
“Ninajisikia vizuri sana nimekua nikisubiri huduma hizi, nilipata meseji kwenye simu yangu nikasema lazima nifike, kwakweli nasubiri nipate huduma hapa, lakini pia naishukuru Serikali kwa kuleta huduma hii kwani wenye matatizo tupo wengi sana: amesema Hussina Mauld Mkazi wa Bangwe.