WANANCHI WAHIMIZWA KUWAPELEKA WATOTO HOSPITALI KUFANYA UCHUNGUZI WA KIFUA KIKUU
Posted on: July 29th, 2025
Wananchi watakiwa kuwapeleka watoto hospitali kufanya uchunguzi wa Kifua Kikuu ili kusaidia kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo kwa watoto wadogo ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha wagonjwa wa kifua kikuu wanapungua Zaidi na kutokuwepo kabisa ifikapo 2030.
Akizungumza katika kipindi cha Morning Jam cha Kicora Fm Bw. Maulid Ntahondi msimamizi na mratibu wa Kifua kikuu ngazi ya jamii kanda ya magharibi amesema wananchi wengi hawafiki vituo vya afya kwa ajili ya uchunguzi wa Kifua Kikuu, ambapo amewakumbusha wananchi kuchukua hatua ya kufanya uchunguzi wa kifua kikuu ili kuweza kuhakikisha kifua kikuu linabaki tatizo la kihistoria katika Mkoa wa Kigoma na Tanzania kwa ujumla.
“katika maandiko imeandikwa watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa sasa hili linatupata katika jamii ambapo watu wengi hawachukui hatua za kuchunguza afya zao pindi waonapo dalili za kifua kikuu hivyo mimi niwaombe wananchi wote wafike katika vituo vya afya kufanya uchunguzi” amesema Ntahondi mratibu wa Kifua kikuu kanda ya Magharibi.
Hata hivyo akitoa ufafanuzi wa kitaalam kuhusu kifua kikuu Dkt. Sylivia Ulio Daktari kutoka kitengo cha magonjwa ya ndani Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni – Kigoma amesema kuwa jamii inapaswa kujua kinga ya mtoto ipo chini hivyo lazima umakini wa kumkinga mtoto na maambukizi ya kifua kikuu uwe wa hali ya juu, kila mzazi anatakiwa kuhakikisha anamkinga mtoto na maambukizi.
“lazima wazazi wawe makini katika kumkinga mtoto na maambukizi ya Kifua Kikuu ambapo kwanza lazima watu wanao mzunguka wasiwe na dalili za Kifua Kikuu lakini pia lazima unapokohoa uhakikishe unaziba mdomo ili kumkinga mtoto na maambukizi” amesema Dkt. Sylivia.
Pia Dkt. Sylivia amebainisha njia mbalimbali za maambukizi ya Kifua Kikuu ambapo amesema njia ya hewa ni moja ya njia ya maambukizi ya Kifuu Kikuu, amesema kuwa watoto, wazee pamoja na waathilika wa VVU wanaweza kuwa hatalini Zaidi kuweza kupata maambukizi ya Kifua Kikuu kwa sababu ya kinga zao kuwa chini ambapo ametoa wito kwa wazazi kuhakikisha wanawafikisha watoto katika vituo vya afya ili kuweza kupata chanjo ambayo hutolewa mapema mala tu matoto anapo zaliwa.
“Kwanza jamii inatakiwa kujua wazee, watoto na wale wenye maambukizi ya VVU wakohatalini Zaidi kupata maambukizi ya Kifua Kikuu hivyo ni jambo la msingi kwa wazazi kuwafikisha watoto kwenye vituo vya afya ili kuweza kupata chanjo ambayo hutolewa baada ya mtoto kuzaliwa” amesema Dkt. Sylivia.
Akizungumza katika kipindi hicho Uwezo Ahmad ameeleza jinsi ambavyo aliona dalili za kuwa na maambukizi ya Kifua Kikuu akiwa na umri wa miaka 16, mwanzo hakujua kama ni dalili za Kifua Kikuu hali ambayo ilipelekea familia yake kukata tamaa na kuhusisha dalili hizo na imani za kishirikina, hata hivyo baada ya kufikishwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni –Kigoma alibainika kuwa na maambukizi ya Kifua Kikuu na kuanza matibabu mala moja jambo ambalo limemsaidia kupona ugonjwa huo.
“Mimi nilianza kuona nakohoa kikohozi chenye mchanganyiko wa damu na baba alivyoona hali ile aliniuliza umekula nini nikamwambia sijala kitu, basi hali hiyo iliendelea kwa muda na familia ilikata tamaa na kudhani kuwa nimelogwa lakini baada ya kufika Maweni nilipima nikagundulika nina maambukizi ya Kifua Kikuuu nilianza dawa mala moja na sasa niko vizuri sina ugonjwa tena” amesema Uwezo.