MAWENI RRH YATOA DAWA BURE KWA WAZAZI WA WATOTO WENYE SELIMUNDU
Posted on: September 24th, 2024Leo tarehe 24 mwezi huu wa tisa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni -Kigoma imeendesha kikao na wazazi wa Watoto wenye ugonjwa wa selimundu (Sickle Cell) kikao ambacho kimetumika kuwaelimisha wazazi pamoja na kutoa dawa bure aina ya (Folic Acid) zinazo tumika kuongeza wingi wa damu kwa mgonjwa.
Katika kikao hicho wazazi wamepata wakati wa kueleza namna mbalimbali ambavyo wangependa Serikali ifanye ili kuweza kuendelea kutoa huduma bora kwa wagonjwa wenye ugonjwa huo wa selimundu.
Mameritha Philipo ambaye ni mzazi wa mtoto mwenye ugonjwa wa selimundu ameiomba Serikali kutafta wadau wanaoweza kusaidia upatikanaji wa matibabu kwa gharama nafuu kwa kuzingatia hali ya Maisha ya sasa,
“Naiomba Serikali yetu iangalie njia ya kuweza kutusaidia sisi wenye maisha ya chini ambao watoto wetu ambao hawawezi kupata matibabu ya kupandikizwa uloto kwa sababu hata haya matibabu ya dawa bado yako juu”amesema Mameritha.
Kwa upande wake Mtaalamu wa Maabara Felix Muzambele amesema kuwa wazazi wanatakiwa kufika hospitalini kupima kwa sababu wapo wagonjwa wengi ambao wako majumbani na hawajulikani kama wanaugonjwa huo bali familia zinawatenga na kuhusianisha ugonjwa hu una Imani za kishirikina.
“Tunawaomba wazazi waache kuhusianisha ugonjwa wa selimundu na imani za kishirikina kwani wagonjwa wa Selimundu hawapaswi kunyanyapaliwa au kutengwa na jamii cha msingi wazazi wawalete Watoto hospitali wapate matibabu” ,amesema Felix Muzambele.