KITUO CHA M-MAMA CHAZINDULIWA MAWENI RRH KIGOMA

Posted on: July 14th, 2023

KITUO CHA M-MAMA CHAZINDULIWA KIGOMA

Kituo cha kuratibu Mfumo wa Huduma ya Usafiri wa Dharura kwa wajawazito, Wazazi na watoto wachanga (m-mama) kimezinduliwa mkoani Kigoma na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Jesca Lebba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.

Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi huo iliyofanyika katika Hospitali ya Mkoa wa Kigoma Maweni, Dkt. Jesca Lebba amewataka watendaji watakaohusika na uendeshaji wa mfumo huo kutanguliza uzalendo kwani ufanisi wake utachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo kwa wajawazito, wazazi na watoto.

Amesema mkoa unauhitaji wa magari 50 kwa ajili ya kusafirisha wagonjwa , yaliyopo kwa sasa ikiwa ni 24 huku upungufu ikiwa magari 26 sawa na asilimia 52.

Upande wake Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Kigoma Dkt. Stanley Binagi amesema ukosefu wa usafiri wa uhakika umekuwa ni changamoto iliyosababisha vifo vingi kwa makundi hayo hivyo ujio wa mfumo huo utapunguza kwa kiasi kikubwa hatari ya vifo kwa wanawake na watoto.

Ameendelea kusisitiza kuwa, kwa kushirikiana na wadau wa Huduma ya m-mama, watahakikisha Mfumo unafanya kazi wakati wote na kwa ubora kutokana na Hospitali kupokea na kutoa huduma kwa wagonjwa wote wanaopewa rufaa kutoka Hospitali za wilaya mkoani Kigoma.

‘’Ili kutimiza malengo ya kuanzishwa mfumo wa m-mama, watendaji wanapaswa kushirikiana na kuhakikisha mfumo unakuwa wazi kiutendaji kwa Saa 24 kila siku ili uweze kutoa huduma nyakati zote’’amesema Dkt. Binagi.

Mfumo wa m-mama unaendeshwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau ambao ni Vodacom, Touch Foundation pamoja na Pathfinder International.