HOSPITALI YA RUFAA MAWENI YAPOKEA MSAADA KUTOKA VODACOM
Posted on: October 9th, 2024
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni – Kigoma imepokea msaada wa vitu mbalimbali kutoka kampuni ya mawasiliano ya VODACOM ikiwa ni maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja, na kupata nafasi ya kutembelea maeneo mbalimbali ya huduma yakiwemo kituo cha mkono kwa mkono (GBV) na Wodi ya wazazi.
Vodacom wametoa vitu hivyo zikiwemo nguo kwa ajili ya wahanga wa ukatili wa kijinsia wanaofika kupata huduma wakiwa na uhaba wa nguo, pia sabuni za unga za kufanyia usafi, taulo za kike, vinywaji mbalimbali kwa ajili ya wodi ya Watoto na vingine vingi ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuhakikisha utoaji wa huduma bora kwa watanzania.
Maofisa kutoka kampuni hiyo ya Vodacom wamepata nafasi ya kuzungumza na Mganga Mfawidhi wa Hospitali Dkt. Stanley Binagi ambapo suala la Voda Bima limechukua nafasi, kwa lengo la kuwasaidiwa wagonjwa wanaopata matibabu hospitalini hapo.
“Napenda kujua kuhusu Voda Bima ni jinsi gani ambavyo tunaweza tukawasaidia wagonjwa ili kuweza kupata huduma lakini pia ni jambo zuri kama mtatusaidia kwa sababu bado tunachangamoto kwenye utoaji wa huduma katika kitua chetu cha mkono kwa mkono (GBV) na kama voda bima inaweza kutumia itakua vizuri “amesema Dkt. Binagi.
Pia maofisa hao kutoka kampuni ya Vodacom wamefika katika kituo cha mkono kwa mkono (GBV) katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni Kigoma pamoja na wodi ya wazazi ambapo wameahidi kuendelea kushirikiana na Hospitali katika kufanikisha wanchi wa Mkoa wa Kigoma wanapata huduma bora.
Hata hivyo Mganga Mfawidhi wa Hospitali Dkt. Stanley Binagi ameishukuru kampuni ya Vodacom kwa msaada ambao wameweza kuutoa na kuichagua Hospitali ya Maweni kuwa sehemu yao ya kurudisha kwa jamii katika maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja ambapo ameiomba kampuni hiyo kuendelea kushirikiana na Hospitali ili kuendelea kutoa huduma bora.