BODI YA USHAURI YAKAA KUJADILI MWENENDO WA HOSPITALI WA ROBO YA PILI
Posted on: February 3rd, 2026Bodi ya Ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni – Kigoma imefanya kikao chake cha robo ya pili ya Oktoba mpaka Desemba, 2026 kikiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo Bw. Lucas Machibya kikiwa na lengo la kujadili mambo mbalimbali ikiwemo taarifa ya fedha ya Robo ya pili ya 2025/2026.
Katika kikao hicho pia taarifa ya utoaji wa Huduma za Afya katika Robo ya pili, 2025/2026 na mapendekezo ya gharama za uchangiaji wa huduma imejadiliwa pamoja na taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Robo hiyo.
Akiwasilisha taarifa ya utoaji wa Huduma za Afya Kaimu Mratibu wa Huduma za Afya Dkt. Yusuph Yagaza amesema katika Robo hiyo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni – Kigoma imeweza kuhudumia wagonjwa 27,388 ikiwa huduma za dharura zimetolewa kwa wagonjwa 1600 ambapo 82% ni watu wazima na %17.1% wakiwa watoto.
“Katika Robo hii tumeweza kuhudumia wananchi 27,388, lakini pia tumeweza kutoa na kupokea rufaa mbalimbali 1,093 sawa na wastani wa rufaa 365 kwa Mwezi na 13 kwa siku pamoja na kinamama wanaojifungua 434 jambo ambalo limeonesha ongezeko la utoaji wa huduma kwa wananchi kulinganisha na robo iliyopita” Dkt Yagaza.
Katika kikao hicho Kaimu katibu wa kamati ya mipango ya Hospitali Muhandisi Lydia Frednand amesema idara mbalimbali zimetekeleza shughuli zilizopangwa katika Robo ya Pili ya 2025/2026 ambapo ametaja idara ya Utawala, upasuaji, pamoja na famasi zimeweza kutekeleza shughuli mbalimbali ambazo zilipangwa kutekelezwa katika Robo hiyo huku akisema Hospitali kwa ujumla ilipanga kutekeleza shughuli 65 ambapo mpaka sasa zimetekelezwa 43 huku 22 zikiwa hazijatekelezwa ikiwa ni sawa na 34%
Hata hivyo Bodi hiyo imeushauri uongozi wa Hospitali kuunda timu ya wataalamu kwenda kujifunza katika Hospitali mbalimbali ambazo zimekua zikifanya vizuri katika utoaji wa baadhi ya huduma ili kuweza kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi, akichangia Hoja Muhandishi, Narcis Choma ambaye ni mjumbe wa Bodi amesema ipo haja ya wataalumu kwenda kujifunza ili kuendelea kuboresha huduma.
“Kama uongozi lazima tufanye jitahada za kuona namna gani tunaweza kuendelea kuboresha huduma hivyo lazima watu wakajifunze ili tupate ujuzi kutoka katika hospitali zingine ambazo zimekua zikifanya vizuri pia hii itatusaidia sana” amesema Choma.



